.


  Hukmu ya asiyetowa Zaka

  Share
  avatar
  Admin
  Admin

  Posts : 22
  Join date : 2010-08-28
  Age : 36
  Location : london

  Hukmu ya asiyetowa Zaka

  Post  Admin on Mon Aug 30, 2010 12:07 pm

  Hukmu ya asiyetowa Zaka

  Kutoa Zaka ni fardhi, na ni katika mambo waliyokubaliana maulamaa wote kuwa yeyote anayeikanusha fardhi hii anakuwa kesha toka katika dini akiwa ni kafiri aliyertadi, isipokuwa kama mtu huyo ni Muislam mpya, na kwa ajili hiyo husameheka kutokana na kutoelewa kwake.

  Ama yule anayeacha kutoa Zaka lakini wakati huo huo hakanushi kuwajibika kwake, huyo anapata dhambi ya kuacha kuitoa, lakini kuacha huko hakumtoi katika dini, isipokuwa ikiwa anaishi katika nchi inayohukumiwa na sheria ya Kiislam, basi anayehukumu atatakiwa aichukuwe Zaka hiyo kwa nguvu.



  Ipo hitilafu baina ya maulamaa iwapo anayeacha kutoa Zaka atozwe gharama kwa kuacha kwake huko kwa ajili ya kumtia adabu, na gharama yenyewe ni kuchukuliwa nusu ya mali yake, na hii inatokana na hadithi iliyotolewa na Imam Ahmad na Annasaiy na Abu Daud na Al Haakim na Al Bayhaqiy kutoka kwa Bahza bin Hakim kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake kuwa amesema:

  "Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) akisema:

  "…Atakayekataa (kutoa Zaka) tutaichukuwa (kwa nguvu, na pia tutachukua) pamoja na nusu ya mali yake haki katika haki ya Mola wetu Mtukufu na watu wa Aali Muhammad si halali kwao kuchukuwa chochote katika hiyo (Zaka)".

  Amesema Imam Ahmed kuwa isnadi ya hadithi hii ni sahihi na amesema Al Hakim kuwa hii ni hadithi sahihi.



  Hata hivyo wapo baadhi ya maulamaa walioidhoofisha hadithi hii na wengine wakasema kuwa hukmu hii ilifutwa baadaye, wakiegemea baadhi ya hadithi zinazoelezea juu ya baadhi ya watu waliochelewa kulipa Zaka na Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) hakuwachukulia nusu ya mali zao.

  Ama ikiwa watu watakataa kutoa Zaka wakiwa wanaelewa kuwa ni jambo la wajibu, na ikiwa zipo nguvu za kuweza kupambana nao, basi watapigwa vita mpaka wakubali kuitoa. Na hii inatokana na hadithi iliyosimuliwa na Bukhari na Muslim kuwa Abdillahi bin Umar (Radhiya Llahu anhu) amesema kuwa Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam) amesema:

  "Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahad ya; Laa ilaaha illa Llah Muhammadan Rasulu Llah, na wasimamishe Swala na watowe Zaka. Wakishafanya hivyo, damu yao na mali zao zitakingika kwangu isipokuwa katika kulipa haki za Kiislam, na hesabu yao iko kwa Mwenyezi Mungu".



  Imeelezwa na Abu Huraira (Radhiya Llahu anhu) kuwa; Alipofariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) na Abubakar akawa (Khalifa), baadhi ya waarabu walikataa kutoa Zaka, na Abubakar (Radhiya Llahu anhu) alitayarisha jeshi akupambana nao.

  Umar akasema (kumuuliza Abubakar):

  "Vipi unataka kupigana vita na watu (Waislam), wakati Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam) alisema:

  "Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahada ya; Laa ilaaha illa Llah na atakayetamka hayo itakingika kwangu mali yake na nafsi yake isipokuwa katika haki yake (anayodaiwa au kisasi kwa makosa aliyofanya), na hesabu yake iko kwa Mwenyezi Mungu?”

  Abubakar (Radhiya Llahu anhu) akasema:

  "Wallahi nitampiga vita yeyote atakayetenganisha baina ya Swala na Zaka, kwa sababu Zaka ni katika 'haki yake' (shahada hiyo). Wallahi lau kama wataacha kunipa mbuzi mdogo (na katika riwaya nyingine 'Kamba') iliyokuwa ikilipwa wakati wa Mtume (Swalla Llahu alayhi wa sallam), ningewapiga vita kwa kukataa kwao kuitoa".

  Umar (Radhiya Llahu anhu) akasema:

  "Wallahi nilipoona kuwa Mwenyezi Mungu amemfungulia Abubakar kifua chake aamue kuwapiga vita, nikajuwa kuwa yuko katika haki".

  Muslim - Abu Daud - na Attirmidhy na maimamu wengine wa hadithi.

   Current date/time is Fri Jan 18, 2019 1:31 pm