.


  Ayaat Madhluumah’ (Aya zilizodhulumiwa).

  Share
  avatar
  Admin
  Admin

  Posts : 22
  Join date : 2010-08-28
  Age : 36
  Location : london

  Ayaat Madhluumah’ (Aya zilizodhulumiwa).

  Post  Admin on Mon Aug 30, 2010 12:46 pm

  Kwa hekima gani Malaika waliuliza?

  Kwa hekima gani Malaika waliuliza?  Mwenyezi Mungu Anasema:  وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلائِكَةِ إِنِّي جَاعِلٌ فِي الأَرْضِ خَلِيفَةً قَالُوا أَتَجْعَلُ فِيهَا مَنْ يُفْسِدُ فِيهَا وَيَسْفِكُ الدِّمَاءَ وَنَحْنُ نُسَبِّحُ بِحَمْدِكَ وَنُقَدِّسُ لَكَ قَالَ إِنِّي أَعْلَمُ مَا لا تَعْلَمُونَ

  “Na pale Mola wako Mlezi Alipowaambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakayefanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa Zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyoyajua” Al Baqarah : 30  Maadui wa Kiislamu wakasema kuwa eti hapa Malaika wanambishia Mwenyezi Mungu, wakasahau kuwa kumbishia Mwenyezi Mungu si kitendo cha kuasi tu, bali ni kitendo cha kufru kubwa mfano wa kitendo cha Iblisi aliyelaaniwa.

  Sisi tunasema kuwa msijaribu kuwakanganya watu, kwa sababu Malaika hawawezi kufanya kitendo cha kumbishia Mwenyezi Mungu, kwani wao wameumbwa kwa ajili ya kutii tu, na wamekingwa na kufanya uasi wa aina yoyote ile.

  Mwenyezi Mungu Amesema juu yao:  لا يَعْصُونَ اللَّهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ

  “Hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa Anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa”. At-Tahriym. 6  Na Akasema:  وَمَنْ عِندَهُ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَلَا يَسْتَحْسِرُونَ يُسَبِّحُونَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَلَا يَفْتُرُونَ

  “Na walioko Kwake hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki. Wanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei” Al-Anbiyaa: 19 -20  Na Akasema:  بَلْ عِبَادٌ مُّكْرَمُونَ لَا يَسْبِقُونَهُ بِالْقَوْلِ وَهُم بِأَمْرِهِ يَعْمَلُونَ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يَشْفَعُونَ إِلَّا لِمَنِ ارْتَضَى وَهُم مِّنْ خَشْيَتِهِ مُشْفِقُونَ

  “Bali hao (wanaowaita wana) ni watumwa waliotukuzwa. Hawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri Zake.Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawamwombei yeyote ila yule Anayemridhia Yeye, nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea.” Al-Anbiyaa: 26-28  Na Akasema juu yao:  يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ  “Vinamkhofu Mola wao Mlezi Aliye juu yao, na vinafanya vinavyoamrishwa.” An-Nahl: 50  Ikiwa hii ndiyo hali yao, na zile ndiyo sifa zao, na kwamba hawamuasi Mola wao, itakuwaje basi waibishie amri ya Mola wao aliyewaumba na kuikanusha hekima ya Mola wao? Kisha wajifanye wanajua zaidi kupita Mola wao? Haiwezekani kabisa kwao kutenda hayo.  Huenda ikawa hekima ya Malaika wale kumuuliza Mola wao juu ya kiumbe kile na vizazi vyake ni kutaka kujua uhusiano utakaokuwa baina yao na viumbe vile, hasa kwa vile mara baada ya kuumbwa kiumbe kile, Malaika waliamrishwa kumsujudia.  Na Mwenyezi Mungu Alijaalia pia wakati ule kuwepo Malaika wote wakubwa kama vile Wenye kuhifadhi na Wenye kuandika na Malaika wa wahyi na wa mvua na wa adhabu na wa mauti…. Wote hawa watakuwa na uhusiano wa daima na kiumbe huyu mpya katika maisha yake yote kwa ujumla.  Suali lao halikuwa na maana ya kupinga au kubisha au kukataa, hasa tukitambua kuwa kumbishia Mwenyezi Mungu ni kufru aliyoifanya Ibilisi aliyelaaniwa.

  Waliuliza kwa sababu hawakuilewa hekima ya kuumbwa kiumbe hiki kipya, kwa hivyo wakataka kujuwa; kwa nini Allaah Anaumba kiumbe kingine? Je wao walipunguza haki yoyote katika amri za Mwenyezi Mungu ndiyo sababu iliyomfanya Mwenyezi Mungu Akataka kuumba kiumbe kingine?

  Hapo ndipo walipouliza kwa kutaka kujua.  Kwa vile hata kabla ya kuumbwa binaadamu huyo, Malaika waliitaja sifa yake kuwa atafanya uharibifu, huenda ikawa ni kwa sababu Mola wao keshawajulisha hayo.

  Pengine walielewa kuwa; kwa vile kiumbe huyu ameumbwa kwa udongo na ataishi juu ya ardhi, bila shaka watakuwa na tabia ya kheri na shari, na kwa ajili hiyo bila shaka yatatokea mapambano baina yao, na uharibifu na ufisadi.  Lakini pale Malaika walipojulishwa sababu ya kuumbwa kiumbe huyo na walipotambua namna Mwenyezi Mungu Alivyompa uwezo wa kupata maarifa na elimu, walimsujudia sajdah ya heshima na kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala).


  Je, Ibilisi alikuwa Malaika?  Mwenyezi Mungu Anasema:  وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلاَئِكَةِ اسْجُدُواْ لآدَمَ فَسَجَدُواْ إِلاَّ إِبْلِيسَ أَبَى وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ  “Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipo kuwa Iblis, alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri." Al Baqarah: 34  Hata aya hii wakaifanya kama ni dalili nyingine ya kuwababaisha watu kuwa eti Malaika wanafanya maasi.  Wakasema kuwa eti Ibilisi ambaye ni Malaika! Hakufuata amri ya Mwenyezi Mungu. Ibilisi aliyepinga alipokisia baina yake na baina ya Adam kwa akili yake iliyofisidika akasema:  أَنَاْ خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ  “Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, naye umemuumba kwa udongo” Al-’Aaraaf : 12  Kwa ajili hiyo akastahiki kutolewa katika rehma ya Mwenyezi Mungu na Pepo Yake. Kama ilivyokuja katika aya nyingi ndani ya Qur-aan Tukufu.  Kwa hivyo tunasema; na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuleta tawfiyq kuwa; Mwenye kudai kuwa Ibilisi alikuwa Malaika, huyo amepotea, na hakuifahamu Qur-aan vizuri, na hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta’ala) keshatoa uamuzi Wake katika kadhia hii, na haijuzu kutanguliza kauli ya mwanadamu mbele ya kauli ya Mwenyezi Mungu au Mtume Wake (Swalla Llaahu ‘alayhi wa sallam). Na haya yanapatikana katika Suratul-Kahf aliposema:  وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ فَفَسَقَ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِ أَفَتَتَّخِذُونَهُ وَذُرِّيَّتَهُ أَوْلِيَاء مِن دُونِي وَهُمْ لَكُمْ عَدُوٌّ بِئْسَ لِلظَّالِمِينَ بَدَلاً  “Na Tulipowaambia Malaika: Msujudieni Aadam! Walimsjudia isipokuwa Iblisi. Yeye alikuwa miongoni mwa majini, na akavunja amri ya Mola wake Mlezi. Je! Mnamshika yeye na dhuriya zake kuwa marafiki badala yangu, hali wao ni adui zenu? Ni ovu mno badala hii kwa wenye kudhulumu.” Al Kahf: 50.  Baada ya ukweli huu ulio wazi usiopingika, mtu anaweza tena kusema kuwa eti Ibilisi ni katika Malaika? Au anaweza kuzirudia zile kauli za Israiliyaat kuwa Ibilisi alikuwa Tausi wa Malaika na mwenye elimu kupita Malaika wote na mcha Mungu kupita Malaika wote na maneno mengine ya mfano huo?  Itakuwaje, wakati Ibilisi amekhitilafiana na Malaika kwa maumbile na tabia na mwanzo na mwisho na katika uhai na katika mwelekeo!  Kuna kushabihiana gani baina ya Ibilisi na Malaika? Wakati wao wameumbwa kwa nuru na yeye ameumbwa kwa moto? Wao hawamuasi Mola wao na wanafanya wanavyoamrishwa, wakati yeye amepinga amri ya Mola Wake na kuibishia hukumu ya Mola Wake. Wao hawaoi wala hawazai, wakati yeye anaoa na anao watoto, wakiwa upande wa maadui wa Mwenyezi Mungu.  Wao ni viumbe wasiofanya kiburi wakaacha kumuabudu Mola wao na wala hawachoki, wakati yeye alikataa na akajivuna na akawa miongoni mwa makafiri. Wao ni wenye kumtakasa Mola wao usiku na mchana, wala hawanyong'onyei, wakati yeye hima yake yote ni kwapoteza waja wa Mwenyezi Mungu, baada ya kuapa kwa utukufu wa Mwenyezi Mungu kuwa atawapoteza watu wote isipokuwa wale asioweza kuwafikia katika watu wema. Na yeye ni yule asiyeiacha njia yoyote wala mlango wowote wa kuwapoteza viumbe isipokuwa ataufuata na kuingia kwa ajili ya kuwafikia.  Mwenyezi Mungu Anasema:  قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ثُمَّ لآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ

  وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَآئِلِهِمْ وَلاَ تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ

  “Akasema: Kwa kuwa umenihukumia upotofu, basi nitawavizia katika Njia yako Iliyonyooka. Kisha nitawazukia mbele yao na nyuma yao na kuliani kwao na kushotoni kwao. Wala hutawakuta wengi wao wenye shukrani” Al-A’araf: 16-17.  Tofauti zote hizi zilizotajwa baina ya Malaika na Ibilisi zinamfanya Ibilisi asiweze kuwa Malaika hata kidogo, tukiongezea ile hukmu Aliyoitoa Mwenyezi Mungu juu yake Aliposema:  قَالَ اخْرُجْ مِنْهَا مَذْؤُوماً مَّدْحُوراً لَّمَن تَبِعَكَ مِنْهُمْ لأَمْلأنَّ جَهَنَّمَ مِنكُمْ أَجْمَعِينَ  “Akasema: Toka humo, nawe umekwisha fedheheka, umekwisha fukuzwa. Hapana shaka atakaye kufuata miongoni mwao, basi nitaijaza Jahannam kwa nyinyi nyote.”

  Al-A’araf: 18.  linabakia suala moja, nalo ni kuwa; Ikiwa Ibilisi si Malaika pana hekima gani iliyojificha hata Mwenyezi Mungu Akasema , “wakamsujudia wote isipokuwa Ibilisi?”  Tunasema; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuleta tawfiyq; hii katika Lugha ya Kiarabu inaitwa ‘istithnaa munqati’a’, (kielezi kilichokatika), na mfano wake kama wanavyosema wataalamu wa Lugha kuwa mfano mtu anaposema: ‘Walikuja wote isipokuwa punda,’ au; ‘Akayala matufaha yote isipokuwa chungwa.’ Na pakasemwa; ‘wakamsujudia wote isipo kuwa Ibilisi’.  Kwa hivyo tunasema; Malaika walipewa amri ya kumsujudia Aadam, na Ibilisi alikuwa pamoja nao (lakini hakuwa mmoja wao – hakuwa mwenzi wao – hakuwa Malaika kama wao), kama tulivyoona katika dalili mbali mbali, na kwa vile wakati ule alikuwa pamoja na Malaika, na alikuwa peke yake miongoni mwa Malaika wengi, ikambidi na yeye asujudu pia, lakini alikataa kwa sababu asili yake kwa kuwa yeye ameumbwa kwa moto na hakuumbwa kwa nuru kama walivyoumbwa Malaika, asili yake ikamzidi nguvu, akaanza kukisia na kupima akajifadhilisha, na matokeo yake akaangamia. Ndiyo maana akapata laana ya Mwenyezi Mungu na ya watu wote.
  Ulikuwaje wasiwasi wa Ibilisi?  Mwenyezi Mungu Anasema:

  وَقُلْنَا يَا آدَمُ اسْكُنْ أَنتَ وَزَوْجُكَ الْجَنَّةَ وَكُلاَ مِنْهَا رَغَداً حَيْثُ شِئْتُمَا وَلاَ تَقْرَبَا هَـذِهِ الشَّجَرَةَ فَتَكُونَا مِنَ الْظَّالِمِين فَأَزَلَّهُمَا الشَّيْطَانُ عَنْهَا فَأَخْرَجَهُمَا مِمَّا كَانَا فِيهِ وَقُلْنَا اهْبِطُواْ بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ وَلَكُمْ فِي الأَرْضِ مُسْتَقَرٌّ وَمَتَاعٌ إِلَى حِينٍ

  “Na tulisema: Ewe Aadam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani, na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale waliodhulumu. Lakini Shaytwaan aliwatelezesha hao wawili na akawatoa katika waliyokuwamo, na tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Katika ardhi yatakuwa makaazi yenu na starehe kwa muda.” Al-Baqarah: 35-36.  Aya hii ilifahamika vibaya kutokana na hadithi za Israiliyaat (zilizosimuliwa na watu wa bani Israil kama walivyonukuu ndani ya Taurat). Imepokelewa katika riwaya za Israiliyaat maelezo ya mti aliokula tunda lake Aadam (‘Alayhis Salaam) kuwa ni mti wa ngano au mzabibu au tini nk.  Na imepokelewa pia katika Israiliyaat juu ya maelezo ya wasiwasi wa Ibilisi kwa Aadam kuwa hakuweza kumtia wasiwasi mpaka alipofanikiwa kuingia ndani ya mdomo wa nyoka, na nyoka wakati huo alikuwa na miguu mine mfano wa ngamia.

  Imepokelewa katika Israiliyaat pia kuwa;

  Na Ibilisi alipoingia Peponi pamoja na nyoka huyo alifanikiwa kumbabaisha Hawwaa na Hawwaa akaweza kumbabaisha Aadam!! Wote wawili wakala tunda, wakajikuta wako uchi, Aadam akajificha ndani ya mti, na Mwenyezi Mungu Akawa Anaita:”Uko wapi ewe Aadam.!!!”

  Aadam akasema: “Nakuonea haya ewe Mola wangu kwani mimi niko uchi.” Akamuambia: “Isije kuwa umekula lile tunda nilokukataza?”  Mwenyezi Mungu Akamkasirkia nyoka yule aliyeingia Ibilisi ndani ya mdomo wake akamuambia: “Umelaaniwa wewe. Kuanzia leo miguu yako ni tumbo lako. Utasota juu ya ardhi na chakula chako kitakuwa ndani ya udongo, na uadui baina yako na wanadamu utakuwa wa milele.”

  Kisha akamuangalia Hawwaa akamuambia: “Umelaaniwa wewe, umembabaisha mja wangu Aadam akala tunda la mti nilomkataza asile, kuanzia leo utabeba mimba kwa dhiki, na hutozaa mpaka utakapoyaona mauti mbele yako.”  Ukweli ni kuwa kilichotangulia ni mojawapo ya visa vya Israiliyaat vilivyonukuliwa katika Taurat iliyobadilishwa na kugeuzwa.. Hapana ndani ya Qur-aan dalili yoyote kuwa Hawwaa ndiye aliyembabaisha Aadam, na wala hapana mahali popote alipotuhumiwa Hawwaa, bali Mwenyezi Mungu Amesema:  فَأَكَلَا مِنْهَا  “Basi wakaula wote wawili.” Twahaa: 120.  Wote wawili kwa pamoja walikula.  Na ili Ibilisi aweze kuwababaisha Aadam na Hawwaa haikuwa lazima kwake aingie Peponi kupitia ndani ya mdomo wa nyoka au wa mnyama yeyote, kwa sababu ili kuingiza wasiwasi hapana lazima ya kukaribiana wala kugusana, bali wasiwasi unaweza kufanyika kwa mbali na kwa karibu pia.  Na nyoka huyu yuko vile vile tokea Alipoumbwa na Mwenyezi Mungu, hakuwa na miguu wala kitu cha kusimamia, bali yupo kama Alivyosema Mwenyezi Mungu:  وَاللَّهُ خَلَقَ كُلَّ دَابَّةٍ مِن مَّاء فَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَى بَطْنِهِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَى رِجْلَيْنِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَى أَرْبَعٍ يَخْلُقُ اللَّهُ مَا يَشَاء إِنَّ اللَّهَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

  “Na Mwenyezi Mungu Ameumba kila kinyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo yao, na wengine huenda kwa miguu miwili, na wengine huenda kwa miguu mine. Mwenyezi Mungu Huumba Ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.” An-Nuur: 45.  Kwa hivyo haya yote yanatokana na hadithi za Israiliyaat zilizojaa ndani ya vitabu vya tafsiri ambazo Waislamu lazima watahadharishwe nazo.

   Current date/time is Fri Jan 18, 2019 1:30 pm