.


  JINSI GANI MWANADAMU ANAWEZA KUUREFUSHA UMRI WAKE ?

  Share
  avatar
  Admin
  Admin

  Posts : 22
  Join date : 2010-08-28
  Age : 36
  Location : london

  JINSI GANI MWANADAMU ANAWEZA KUUREFUSHA UMRI WAKE ?

  Post  Admin on Mon Aug 30, 2010 9:14 pm

  Ni watu wangapi waliowafikiwa kutenda amali kubwa na nyingi katika umri mdogo (mchache) mpaka ikadhaniwa kwamba hiyo ni aina ya mambo yasiyo ya kawaida. Ukweli ulivyo si mambo yasiyo ya kawaida, bali hiyo ni baraka ya umri na taufiq ya Allah kwa mja wake. Itoshe kuwa ni kigezo na mfano hai kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Amewafikiwa kuwatoa watu katika viza vya ushirikina na kuwatia katika nuru ya Uislamu, na akaweza kuibadilisha kabisa historia nzima ya mwanadamu mpaka leo na mpaka atakapo Allah. Ameyafanya yote haya katika kipindi kisichopungua miaka ishirini na tatu. Akasimamisha mfumo mpya na sahihi wa maisha (Uislamu), akakilea kizazi cha pekee chini ya mfumo huu na kuasisi uma wenye kupigiwa mfano na dola ya kilimwengu katika kitambo hiki kifupi. Pamoja na vikwazo na magumu yote aliyokumbana nayo tangu siku ya mwanzo ya kazi yake hii, bado alipata mafanikio makubwa haya. Na wala usitoe hoja ukasema: Hakika Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliweza kuyafanya yote hayo kwa sababu alipewa msaada wa miujiza. Nani kama yeye, tu wapi sisi hata tujilinganishe naye?!

  Uhalisia wa mambo ni kuwa maisha ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika ulinganiaji na upiganiaji wake wa dini. Yalikuwa yakifuata kanuni na utaratibu wa Allah wa kawaida (uliozoweleka na kutambuliwa na watu) na wala haikuwa ni miujiza. Hakika si vinginevyo, muijiza huja mahala maalumu, mahala ambapo zimetolewa na kufanywa kila sababu zimkinikazo katika ardhi na haujabakia ila msaada kutoka mbinguni. Ni katika hali na mazingira kama haya ndipo huja msaada wa miujiza. Kama ambavyo Allah alivyompa msaada wake katika suala zima la Hijrah wakati alipomteremshia utulivu wake na kumpa msaada wa majeshi yasiyoonekana. Kadhalika katika vita vya Badri baada ya kufanya sababu zote, hapo ndipo Allah akampa msaada wa malaika alfu moja wenye kufuatana mfululizo: “NA ALLAH HAKUFANYA HAYA ILA IWE BISHARA (khabari ya furaha) NA ILI NYOYO ZENU ZITUE KWAYO...”. [8:10]

  Hebu waangalie makhalifa waongofu na maswahaba wote wa Bwana Mtume-Allah awawiye radhi-na wale wote waliowafuatia katika imani. Waangalie namna gani walivyoufungua ulimwengu, wakaueneza Uislamu, wakayafundisha mataifa, wakayagurisha kutoka katika dini zao za kijahili na ada zao mbaya katika kipindi cha miongo kadhaa tu. Kiasi cha kuwaacha wanahistoria wakiyashangaa mapinduzi haya yaliyofanywa na Uislamu ulimwenguni katika kipindi kifupi mno kuwahi kutokea katika historia nzima ya mwanadamu. Mapinduzi ya kidini, kifikra, maisha binafsi na yale ya kijamii sambamba na mapinduzi ya kisiasa. Hebu muangalie kwa mfano mtu kama Umar Ibn Abdul-Aziyz-Allah amrehemu. Huyu alifanya kila lililo katika uweza wake kuhakikisha kuwa ukhalifa unarudi katika uongofu wake kama ulivyokuwa katika zama za makhalifa waongofu. Aliweka mikakati ya kurejesha haki zilizodhulumiwa kwa wanaozistahiki na amana kwa wenyewe. Aliyafanya yote haya ili isije ikampata mbele ya Allah lawama ya mwenye kulaumu. Katika kipindi kifupi mno cha ukhalifa wake; miaka miwili na nusu tu aliweza kutokana na nia njema aliyokuwa nayo kuijaza ardhi usawa na uadilifu. Allah amuwiye radhi amirul-muuminina Umar Ibn Abdul-Aziyz.

  Uzito wa amali huzidi katika mizani ya haki na hurudufika thamani na thawabu zake mbele ya Allah kila vinapokithiri vikwazo katika njia ya kuitekeleza. Hapa ndipo unapoonekana ubora wa maswahaba juu ya watu waliokuja baada yao. Hii ni kwa sababu wao waliamini wakati ambapo watu walikufuru, wakamsadiki Bwana Mtume katika kipindi ambacho watu wanamkadhibisha na kumpinga. Kadhalika ndivyo ulivyokuwa ubora wa waliotangulia wakawa wa kwanza kuingia katika Uislamu miongoni mwa Muhajirina na Answaari, kwa maswahaba waliowafuatia nyuma yao. Ambao waliosilimu baada ya ‘Fat-hi Makah’ na kudhihiri nguvu na kitisho cha Uislamu. Katika hili Qur-ani Tukufu inasema: “...HAWAWI SAWA MIONGONI MWENU WALE WALIOTOA KABLA YA KUSHINDA (kwa kutekwa Makah) NA WAKAENDELEA KUPIGANA. (Maswahaba) HAO WANA DARAJA KUBWA ZAIDI KULIKO WALE AMBAO WAMETOA BAADAE NA WAKAPIGANA. NA ALLAH AMEWAAHIDIA WEMA WOTE HAO...”. [57:10]

  Kadhalika ni kwa mantiki hii amali njema inayotendwa katika zama ambazo jamii za wanadamu zimefisidika na kufilisika kimaadili. Zama ambazo viongozi/watawala huwa madhalimu, matajiri huishi maisha ya anasa mno, wenye nguvu hutakabari na wanazuoni hujipendekeza kwa watu. Zama ambazo uovu huenea na mambo machafu kufanywa dhahiri shahiri na wema kuadimika. Amali njema katika zama hizi huwa na ujira mkubwa sana na daraja ya juu kabisa. Washika dini katika zama hizi na katika hali na mazingira kama haya ni mithili ya maswahaba wapya, kutokana na kutupwa dini nyuma na kuwekwa mbele ‘Jahilia”. Imethibiti katika hadithi sahihi kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Ibada katika (zama za ghasia za) fitna na ikhtilafu ni kama Hijrah ya kunifuata”. Muslim, Tirmidhiy & Ibn Maajah.

  Imepokewa kutoka kwa Abuu Umayyah As-sha’abaaniy amesema: Nilimuendea Abuu Tha’alabah Al-khashaniy nikamuuliza: Unaifanyaje aya hii? Akasema: Aya ipi hiyo? Nikamwambia: “ENYI MLIOAMINI! LILILO LAZIMA JUU YENU NI NAFSI ZENU. HAWAKUDHURUNI WALIOPOTOKA IKIWA MUMEONGOKA...” [5:105] Akaniambia: Nilimuuliza kuhusiana nayo (aya hiyo) mjuzi wa mambo, nilimuuliza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Bali jiamrisheni kufanya mema na jikatazeni maovu mpaka utakapoona ubakhili unatiiwa, matamanio ya nafsi yanafuatwa, dunia inapendwa zaidi (kuliko akhera) na kila mwenye rai kupendezwa na rai yake. Na utapoona huna uwezo wa kuamrisha (ukatiiwa, basi wakati huo ndio) jilazimishe na yanayoikhusu nafsi yako (tu). Hakika mbele yenu kuna siku za subira, kusubiri ndani ya siku hizo ni mithili ya kukamata kaa la moto. Mwenye kufanya amali njema ndani ya siku hizo, ana ujira wa mithili ya watu khamsini wanaofanya mithili ya amali yake hiyo”. Ibn Maajah, Tirmidhiy & Abuu Daawoud. Abuu Daawoud akazidisha katika riwaya yake: “Pakasemwa (pakaulizwa) ewe Mtume wa Allah, ujira wa watu khamsini miongoni mwetu sisi (maswahaba wako) au miongoni mwao (watu wa zama hizo)? Mtume akasema: Bali ujira wa watu khamsini miongoni mwenu nyinyi”.

  Bwana Mtume ametaja katika baadhi ya riwaya kuelezea sababu ya urudufu/muongezeko huu wa ujira, akasema: “Hakika nyinyi mnapata wasaidizi katika kufanya kheri na wao hawatampata wa kuwasaidia katika (kufanya amali za) kheri”. Kauli hii ya Bwana Mtume inamaanisha kwamba hadithi hii ilielekezwa kwa baadhi ya maswahaba baada ya kuenea kwa Uislamu na kuingia watu katika dini makundi kwa makundi na kuwepo wanaosaidia katika kheri. Kwani waliotangulia wakawa wa mwanzo kuingia katika dini; miongoni mwa Muhajirina na Answaari, hawakuwa na watu wa kuwasaidia katika kuutekeleza Uislamu wao, hawa hawalingani na ye yote katika ubora. Kadhalika hadithi inawajibisha kuendelea kuamrisha mema na kukataza maovu maadam lipo sikio linalosikia na moyo unaozingatia. Maadam yapo matumaini japo finyu ya kusikilizwa kwa namna moja au nyingine.

   Current date/time is Fri Jan 18, 2019 1:54 pm