.


  KWA HATUA NGAPI ILITEREMSHWA QURANI?

  Share
  avatar
  essam

  Posts : 3
  Join date : 2010-08-28
  Age : 34
  Location : dublin

  KWA HATUA NGAPI ILITEREMSHWA QURANI?

  Post  essam on Sat Aug 28, 2010 9:10 am

  Kwa hekima Zake Mwenyezi Mungu S.W.T. anazojua Yeye Mwenyewe na kwa upendo Wake na elimu Yake, Qur-ani Tukufu iliteremshwa kwa hatua tatu tofauti kama ifuatavyo:

  Kama alivyotuelezea Ibn Abbaas R.A.A. kasema: Hatua ya kwanza kabisa iliteremshwa Qur-ani yote kwa jumla na kuandikwa na kuhifadhiwa kwenye Ubao uliohifadhiwa (Lawhin Mahfuwdh). Lakini hakuna mtu yeyote yule anayefahamu lini iliteremshwa na jinsi ilivyoteremshwa isipokuwa Mwenyezi Mungu S.W.T.. Kama alivyotuhakikishia katika Suratil Buruwj aya ya 21 na ya 22, “

  بَلْ هُوَ قُرْآنٌ مَجِيدٌ * فِي لَوْحٍ مَحْفُوظٍ
  Maana yake, “Bali hii ni Qur-ani Tukufu. (Iliyotolewa) katika huo Ubao uliohifadhiwa, (wa Mwenyezi Mungu).”

  Na hatua ya pili iliteremshwa Qur-ani Tukufu kitabu kamili na Malaika Jibril A.S. kutoka katika Ubao uliohifadhiwa (Lawhin Mahfuwdh) mpaka kwenye mbingu ya dunia mahali panapoitwa Baitul Izza (Nyumba ya Izza) kwa usiku mmoja uliobarikiwa na wenye heshima kubwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, kama alivyouita Yeye Mwenyewe Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Dukhaan aya ya 3, “

  إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُبَارَكَةٍ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ
  Maana yake, “Hakika tumekiteremsha (Kitabu) katika usiku uliobarikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji.”

  Na pia katika Suratil Baqarah aya ya 184, "
  شَهْرُ رَمَضَانَ الذي أنْزِلَ فِيْهِ القُرآنُ
  Maana yake, “Mwezi wa Ramadhani ambao ndio iliteremshwa Qur-ani.”

  Na vilevile katika Suratil Qadr aya ya 1, "
  إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَة القَدْرِ
  Maana yake, “Hakika tumeiteremsha (Qur-ani) katika usiku wenye heshima kubwa (usiku wa mwezi wa Ramadhani).”

  Kisha hatua ya tatu akawa Malaika Jibril A.S. akiiteremsha Qur-ani kidogo kidogo kwa matokeo maaalum kutoka katika mbingu ya dunia mpaka kumfikia Mtume wetu S.A.W. kama nilivyozitaja sababu zake. Kama ilivyopokelewa na Ibn Abbaas R.A.A. katika Hadithi iliyotolewa na Haakim na Bayhaqi kasema, “

  "فضل القرآن من ذكر فوضع في بيت العزة من السماء الدنيا، فجعل جبريل ينزِّل به على النبي ."
  Maana yake, “Imefadhiliwa Qur-ani kuliko ukumbusho (wowote ule). Ikawekwa katika Baitul Izza (Nyumba ya Izza) kwenye mbingu ya dunia. Akawa (Malaika) Jibril akiiteremsha kwa Mtume S.A.W. (kidogo kidogo).”

  Na pia katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Abbaas R.A.A. na kutolewa na Haakim na Bayhaqi kasema, “
  "أنزل القرآن جملة واحدة إلى السماء الدنيا ليلة القدر، ثم أنزل بعد ذلك في عشرين سنة."
  Maana yake, “Imeteremshwa Qur-ani yote kwa pamoja mpaka kwenye mbingu ya dunia katika usiku wa heshima kubwa. Kisha ikateremshwa baada ya hapo kwa miaka ishirini.”

  Na vilevile katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Abbaas R.A.A. na kutolewa Haakim na Bayhaqi kasema, “
  أنزل القرآن جملة واحدة إلى السماء الدنيا ليلة القدر، وكان بمواقع النجوم ، وكان الله ينزله على رسوله 
  ."بعضه في إثر بعض
  Maana yake, “Imeteremshwa Qur-ani yote kwa pamoja mpaka kwenye mbingu ya dunia katika usiku wenye heshima kubwa. Na ilikuwa (kabla ya hapo) katika maangukio ya nyota (mbinguni). Na Mwenyezi Mungu alimteremshia (Qur-ani) Mtume Wake S.A.W. kidogo kidogo.”

   Current date/time is Fri Jan 18, 2019 1:37 pm