.


  Itikadi yetu juu ya Qur'ani tukufu

  Share
  avatar
  essam

  Posts : 3
  Join date : 2010-08-28
  Age : 34
  Location : dublin

  Itikadi yetu juu ya Qur'ani tukufu

  Post  essam on Sun Aug 29, 2010 11:35 am

  Itikadi yetu

  Imam Shafi (Rahimahu Llah) alipoletwa mbele ya Khalifa Haarun Al Rashiyd baada ya kusingiziwa uongo na gavana aliyekuwa akitawala Yemen wakati ule, aliletwa akiwa amefungwa minyororo mpaka shingoni.

  Baada ya kuulizwa masuali mengi na Khalifa huyo akamtaka aelezee nini anachokijuwa juu ya Elimu ya Qurani.

  Imam Shafi (Rahimahu Llah) akajibu:

  “Hakika Elimu za Qurani ni nyingi, je! Unaniuliza juu ya aya zisizobeba isipokuwa maana moja tu (Muhkam) au zinazobeba maana zaidi ya moja (Mutashaabih) au ipi iliyotangulia na ipi iliyokuja baada yake (Taqdiym na Taakhiyr) au unataka kujuwa ipi iliyofutwa na ipi iliyofuta (Nasikh na Mansukh) au juu ya ………?”

  Akaendelea hivyo huku akijibu kila suala analoulizwa na Harun Al Rashiyd mpaka Khalifa huyo alipohakikisha kuwa huyu ni Alim wa kweli na kwamba aliozuliwa ulikuwa ni uongo, akaamua afunguliwe minyororo na apewe heshima zote wanazopewa Maulamaa.  Kwanza ningependa kumhakikishia kila Muislamu kuwa Itikadi yetu ni uwa Qurani hii tukufu tuliyo nayo ndiyo ile ile aliyoteremshiwa Mtume wetu Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na kwamba haijapungua ndani yake wala kuongezeka Sura yoyote au Aya au hata Herufi moja.  Msahafu huu tunaousoma na yale yaliyomo ndani yake ni yale yale yaliyokuwemo tokea wakati Mtume Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alipokuwa akitembea juu ya ardhi hii na akiteremshiwa Wahyi, na hapana mwanachuoni yeyote wa Kisunni aliyewahi kusema kinyume cha haya.  Ningependa kuwahakikishia ndugu zangu Waislamu pia kuwa haya yanayoandikwa ndani ya mitandao siku hizi kuhusu Waislamu kuwa wanasema Qur’ani imepungua, ni mojawapo ya fitna za Manasara (Wakristo) wenye kuudurusu Uislamu kwa ajili ya kuupiga vita, na haya yamejaa katika mitandao yao.

  Nawahakikishia ndugu zangu Waislamu pia kwamba hizo riwaya zinazoandikwa katika mnasaba huu, ni baadhi ya matukio machache sana yaliyotokea wakati wa kukusanya Qur’ani tukufu na kuiandikwa yote katika msahafu mmoja, na haya yalikuwa wakati wa ukhalifa wa Abu Bakar na wakati wa Uthman (Radhiya Llahu anhum). Riwaya hizo za kupotosha zimenukuliwa kabla ya kupatikana Ij’maa juu ya utaratibu wa kuiandika Qurani yote ndani ya msahafu mmoja.

  Na inajulikana na kila Muislamu kuwa alipokuwa akiteremshiwa Wahyi Mtume wetu Muhammad (Swallah Llahu alayhi wa sallam), Qur’ani ilikuwa ikiandikwa na Masahaba (Radhiya Llahu anhum) ndani ya magamba na makozi ya miti na majani nk. Na haikuwa imekusanywa mahala pamoja, katika kitabu kimoja kama ilivyo hivi sasa.

  Kwa ajili hiyo ulikuwepo uwezekano wa baadhi ya Aya kupatikana kwa Sahaba huyu na kukosekana kwa Sahaba mwingine (Radhiya Llahu anhum), na pia ulikuwepo uwezekano wa Sahaba (Radhiya Llahu anhu) kuandika dua zake au hadithi ndani ya karatasi au gamba analoandika Qurani kwa sababu ya kutokuwepo vifaa vya kuandikia wakati ule kama vile karatasi nk..

  Na haya yote kama nilivyotangulia kusema ni kuwa yalitokea kabla ya kupatikana Ij’maa, wakati Masahaba wote kwa pamoja (Radhiya Llahu anhum) walipokubaliana chini ya uongozi wa Khalifa wao Abu Bakar (Radhiya Llahu anhu) kuikusanya Qurani.  Kukusanywa kwa Qur’ani

  Kukusanywa kwa Qur’ani tukufu kulifanyika mara tatu.

  a- Wakati wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam)

  b- Wakati wa Abubakar (Radhiya Llahu anhu)

  c- Wakati wa Othman (Radhiya Llahu anhu).  Wakati wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam) watu walikuwa wakiipenda sana Qurani na kuisoma misikitini na majumbani na walikuwa wakishindana katika kuhifadhi, hata katika baadhi ya riwaya zilizopokelewa zinasema kuwa watu walikuwa wanapofunga ndoa, mahari yao yalikuwa ni Qurani. Walikuwa wakiulizwa; “Umehifadhi Sura fulani?” Na jawabu ikiwa ‘Ndiyo’, basi huambiwa kuwa mahari yake ni kumfundisha mkewe Sura hiyo.

  Na lilikuwa ni jambo la kawaida kama ilivyo sasa ndani ya Swala, Imam anapokosea, hukosolewa na aliye nyuma yake.

  Kwa hivyo wakati wa Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam), Qurani ilikuwa imekwishahifadhiwa vifuani mwa Waislam pamoja na kuandikwa katika magamba, katika majani, makozi, mafupa n.k.

  Isisahaulike pia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliwachagua baadhi ya Masahaba (Radhiya Llahu anhum) na kuwapa jukumu la kuiandika Qurani kila anapoteremshiwa Wahyi, na Masahaba hawa walikuwa wakijulikana kama ni; ‘Kuttabul Wahyi’. Na maana yake ni, ‘Waandishi wa Wahyi’.

  Alikuwa anapoteremshiwa Wahyi, akiwaita na kuwaamrisha kuyaandika yale aliyofunuliwa.  Kwa hivyo Qurani iliandikwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na ilikuwepo kwa baadhi ya Sahaba waliokuwa wakiandika Wahyi, na pia ilihifadhiwa vifuani mwa Waislam. Isipokuwa iliandikwa juu ya magamba na majani na makozi ya miti, nk. Kutokana na kutokuwepo au kwa sababu ya upungufu wa vifaa vya kuandikia. Na haikuwa imekusanywa mahala pamoja, katika kitabu kimoja kama ilivyo hivi sasa.

  Jambo lingine muhimu ni kuwa Qur'ani tukufu iliteremshwa kwa misomo saba, na hii ni baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kumuomba Mola wake afanye hivyo ili waarabu wasiokuwa wa kabila la Qureshi nao waweze kuifahamu vizuri.

  Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) amesema:

  “Jibril alinisomea Qurani kwa herufi (msomo wa aina) moja, nikamwambia aniongezee mpaka ikafikia misomo saba”

  Bukhari na Muslim  Mtume (Swallah alayhi wa sallam) kaihifadhi Qurani yote.

  Jibril (Alayhis Salaam) alikuwa akimsikiliza Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) Qurani yote mara moja kila mwaka, na katika mwaka aliofariki, Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alisikilizwa Qurani yote mara mbili. Na dalili ni hadithi iliyosimuliwa na Imam Muslim kutoka kwa Bibi Aisha (Radhiya Llahu anha) aliposema:

  “Tulikuwa wake wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) sote kwake na hakuna aliyeondoka, na Fatima akaja huku akitembea kwa mwendo wake uliokuwa kama wa baba yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na Mtume alipomuona alimkaribisha na kumwambia:

  ‘Karibu mwanangu’, kisha akamtaka akae kuliani au kushotoni pake, kisha akamnon’goneza, na (baada ya kunon’gonezwa) akalia kilio kikubwa kisha akamnon’goneza tena, na akacheka. Nikamwambia:

  ‘Baba yako amekunon’goneza peke yako mbele ya wake zake wote kisha unalia?’ (badala ya kufurahi)

  Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) aliposimama nikamuuliza:

  ‘Baba yako alikwambia nini?’

  Akanijibu:

  ‘Siitowi siri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu’

  Baada ya kufariki Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), (Fatima) akaniambia:

  ‘Sasa nitakwambia, ama pale aliponinong’oneza mara ya mwanzo (nikalia), aliniambia kuwa; ‘Kwa kawaida Jibril hunisikiliza Qurani yote mara moja kila mwaka lakini safari hii kanisikiliza Qurani yote mara mbili, na sioni tafsiri ya kitendo hicho isipokuwa ni kuwa kifo changu kinakaribia, kwa hivyo mche Mungu na kuwa na subira kwa sababu mimi ni kizazi chema kwako kilichokutangulia.’ Akasema: Ndipo pale mliponiona nikilia, na alipoiona huzuni yangu, akaninon’goneza tena na kuniambia:

  ‘Fatima, hutoridhika ukiwa wewe ni bibi wa wanawake wa Kiislam? Au Bibi wa wanawake wa Umma huu?’

  Akasema: Ndipo nilipocheka pale mliponiona nikicheka”.

  Kutokana na dalili hii, tunatambua kuwa Qurani yote ilikuwa ishahifadhiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kabla hajafariki dunia.

  Masahaba (Radhiya Llahu anhum) walikuwa wakiisoma pia

  Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) alikuwa akiwasomea Masahaba na yeye akisomewa Qurani kwa ajili ya kuwafundisha na kuhakikisha kuwa wameihifadhi kama inavyotakikana.

  Imepokelewa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) siku moja alimtaka Abdillahi bin Masaood (Radhiya Llahu anhu) amsomee Qurani, na akamsomea Suratul Nisaa mpaka alipofika aya ya 41 isemayo:

  فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِن كُلِّ أمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَى هَـؤُلاء شَهِيدًا

  “Basi itakuwaje tutakapoleta shahidi katika kila uma; na tukakuleta wewe (Nabii Muhammad) uwe shahidi juu ya huu (Uma wako)?”

  Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) akamwambia:

  ‘Basi, hapo hapo, inatosha’

  Abillahi bin Masaood anasema:

  ‘Nilipomtizama nikamwona macho yake yanamtiririka machozi’

  Muslim.  Kukusanywa Qur’ani wakati wa Abu Bakar (Radhiya Llahu anhu)

  Kama tulivyoona hapo mwanzo kuwa Qur'ani iliandikwa, ilisomwa, ilikusanywa na kupangwa kama ilivyotakikana chini ya uongozi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), aliyekuwa akifundishwa na Jibril (Alayhis Salaam).

  Lakini haikuwa imekusanywa katika kitabu kimoja kama ilivyo hivi sasa  Katika vita vya Al Yamama vilivyotokea mwaka wa kumi na mbili baada ya Hijra, mwaka wa pili baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) kufariki dunia, Masahaba sabini katika waliohifadhi Qur’ani tukufu waliuliwa na majeshi ya Musailima l kadhaab aliyejidai utume.

  Jambo hili lilimsitua sana Umar bin Khatwaab (Radhiya Llahu anhu) aliyemuendea Abu Bakar (Radhiya Llahu anhu) kumshauri kuiandika na kuikusanya Qurani yote katika kitabu kimoja isije ikapotea kwa sababu ya kufa kwa walioihifadhi na kupotea vifaa vilivyoandikwa ndani yake.

  Abu Bakar (Radhiya Llahu anhu) kwanza alikataa kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) hakuwahi kufanya kitendo hicho, lakini baada ya kushikiliwa na Umar na kumfahamisha juu ya hatari ya kuuliwa Sahaba wengine waliohifadhi na Qur'ani kupotea, akaona kuwa kweli ipo haja ya kufanya hivyo.

  Umar akatangaza kwa kusema:

  “Waandishi wa Wahyi wote waliokuwa wakiandika mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) walete yale waliyoandika”.

  Watu wakauitikia mwito, na Zeyd bin Thabit (Radhiya Llahu anhu) ndiye aliyepewa jukumu la usimamizi na uongozi wa kuifanya kazi hiyo, na hakuwa akikubali kuandika chochote isipokuwa mbele ya mashahidi wawili, mmoja katika waliohifadhi Qur'ani na mwengine katika walioiandika Qur'ani tukufu mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na lazima zikubaliane kila herufi, na alikuwa kabla ya kuandika akipambanisha yale yaliyoandikwa na yale yaliyomo vifuani mwa waliohifadhi, pamoja na kuhakikisha kwa kupambanisha yaliyoandikwa hapo mwanzo na yale yaliyonukuliwa baadaye na watu wengine, yote haya kwa ajili ya kuhakikisha kuwa ananukuu kila herufi kama inavyopaswa.

  Hakutegemea hifdhi ya mtu mmoja, bali alikuwa akifanya tahakiki juu ya kila aya kabla ya kuiandika kwa kuwasikiliza wengi miongoni mwa waliohifadhi.  Kulitokea mabishano baina ya Zeyd na Umar (Radhiya Llahu anhum) katika herufi za و‘Waaw’ katika aya tatu zifuatazo;

  وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَان

  Wa lladhiynat tabauuhum bi ihsanin – na

  وَآخَرِينَ مِنْهُمْ لَمَّا يَلْحَقُوا بِهِمْ

  Wa aakhariyna minhum lamma yal haqku bihim –

  وَالَّذِينَ جَاؤُوا مِن بَعْدِهِمْ

  Wa lladhiyna jaauw min baadihim

  Umar alikuwa akiona kuwa hakukuwa na herufi ‘waaw’ na kwamba aya husomwa;

  Alladhiyna ttabauuhum bi ihsanin – na

  Aakhariyna minhum lamma yal haqu bihim – na

  Alladhiyna jaauw min ba-adihim

  Zeyd alikataa kuziandika kwa rai ya Umar, akasema kuwa aya hizo zinasomwa kwa herufi ya ‘waaw’

  Umar (Radhiya Llahu anhu) akasema:

  ‘Mwiteni Kaab’ (Huyu ni katika waandishi wa Wahyi na pia katika waliohifadhi).

  Akaitwa Kaab (Radhiya Llahu anhu) aliyemuunga mkono Zeyd dhidi ya Umar (Radhiya Llahu anhum), kuwa aya zote hizo husomwa kwa ‘waaw’.  Zeyd (Radhiya Llahu anhu), alikuwa miongoni mwa waandishi wa Wahyi waliohifadhi Qurani, na alikuwa pia katika walioandika aya za mwisho za Qurani mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).

  Anasema Zeyd bin Thabit (Radhiya Llahu anhu), aliyekabidhiwa jukumu hilo la kuikusanya na kuiandika Qur'ani akishirikiana na Masahaba wenzake waliochaguliwa kwa kazi hiyo:

  “Nikaanza kukusanya kutoka katika kila sehemu iliyoandikwa na kutoka kwa watu walioihifadhi vifuani mwao, mpaka nilipoipata aya ya mwisho ya Sura ya At Tawba ikiwa kwa Abi Khuzayma l Ansari peke yake na hakuwa nayo mwengine isipokuwa yeye na aya yenyewe ni:

  لَقَدْ جَاءكُمْ رَسُولٌ مِّنْ أَنفُسِكُمْ عَزِيزٌ عَلَيْهِ مَا عَنِتُّمْ حَرِيصٌ عَلَيْكُم بِالْمُؤْمِنِينَ رَؤُوفٌ رَّحِيمٌ

  “Amekufikieni Mtume alie jinsi moja na nyinyi, yanamhuzunisha yanayokutaabisheni , anakuhangaikieni. (Na) kwa walioamini ni mpole na Mwenye huruma ….”

  Mpaka mwisho wa aya hiyo.”

  Aya hii ilikuwa imehifadhiwa moyoni na wengi, lakini haikuwa imeandikwa pengine isipokuwa kwa Sahaba huyo peke yake.  Baada ya kukusanywa huko, pamoja na kulinganishwa na Qurani iliyoandikwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na hatimaye kuandikwa katika kitabu kimoja, msahafu huo ukawa kwa Abu Bakar (Radhiya Llahu anhu) mpaka alipofariki dunia, kisha ukawa kwa Umar (Radhiya Llahu anhu), na hatimaye ukabaki nyumbani kwa Hafsa bint Umar (Radhiya Llahu anhum).  Kukusanywa Qur'ani wakati wa Uthman (Radhiya Llahu anhu)

  Wakati wa ukhalifa wa Uthman (Radhiya Llahu anhu), dini ya Kiislam ilipata nguvu zaidi, na Waislam waliweza kuzishinda nchi mbali mbali na kusonga mbele kufikia Azarbeijan na Armenia na kuweza pia kuziteka nchi mbali mbali za Asia na Europe.

  Baadhi ya Masahaba kama vile kina Hudhaifa (Radhiya Llahu anhu), wakaona mambo ya kiajabu kila wanaposonga mbele kuziteka nchi hizo. Katika nchi ya Syria na Misri kwa mfano; Waislam walikuwa wakishindana kwa kutamba, kila mmoja akisema kuwa msomo wake wa Qurani (katika ile misomo saba iliyotemshiwa Qur'ani) ni bora kuliko wa mwenzake na kufikia hadi kukufurishana.

  Uthman (Radhiya Llahu anhu) aliposikia hayo, alishauriana na Masahaba wenzake na akaona kuwa ipo haja kubwa sana ya kuwaunganisha Waislam wote wawe wanaisoma Qurani kwa msomo mmoja tu na kwa kutumia herufi moja tu.

  Wakakubaliana Masahaba wote (Radhiya Llahu anhum), kuwa ule Msahafu uliokusanywa na Abubakar (Radhiya Llahu anhu), uchukuliwe na unukuliwe kwa kuuandika tena katika misahafu mingine mingi, na wakakubaliana kuwa itumike lugha ya ki Qureshi ambayo ndiyo iliyoteremshiwa Qurani, kisha waisambaze misahafu hiyo kila pahali katika nchi za Kiislam na kuichoma moto yote iliyobaki iliyoandikwa kwa misomo tofauti.

  Ikachaguliwe tume ya waliohifadhi Qurani pamoja na wajuzi wa lugha na Uthman aliwaambia:

  "Ikitokea hitilafu yoyote juu ya neno lolote basi liandikeni kwa lugha (lahja) ya ki Qureshi’

  Baada ya kazi hiyo kukamilika, Uthman akaurudisha msahafu wa Abubakar nyumbani kwa Hafsa.

  Haya yalifanywa baada ya kupatikana makubaliano baina ya Umma wote kuwa ipo haja kubwa ya kufanya hivyo.  Sayiduna Aly (Radhiya Llahu anhu) alipowasikia baadhi ya watu wakimlaumu Uthman (Radhiya Llahu anhu) kuwa amechoma moto Qur'ani, aliwaambia:

  “Muogopeni Mola wenu enyi watu, na wala msipindukie mipaka katika kumlaumu Uthman kwa kusema kuwa eti yeye ni mchomaji wa misahafu, kwani Wallahi misahafu imechomwa mbele ya Masahaba wote na baada ya kukubaliana sote. Na mimi ningelikuwa kiongozi, basi ningefanya kama alivyofanya”.

  Kwa hivyo Abubakar (Radhiya Llahu anhu) aliikusanya na kuiandika Qurani kwa kuogopa isipotee kwa sababu ya kufa kwa waliohifadhi, lakini Uthman (Radhiya Llahu anhu), aliiandika na kuichoma iliyobaki kwa kuogopa mfarakano.

  Lakini Qurani aloiandika Uthman ni ile ile aloiandika Abubakar, aliyoinukuu kutoka katika ile iliyoandikwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na kuhifadhiwa.

  Mtu anaweza kuuliza:

  ‘Kwa nini Uthman ameacha kukiendeleza kitendo alichofanya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) cha kuisoma Qurani kwa misomo mingi?"

  Jibu:

  Kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), hakuamrisha hivyo, bali alipendekeza tu, kwa sababu wakati ule ilikuwepo haja ya kuwafundisha watu kusoma Qurani kwa misomo yao mbali mbali, lakini wakati wa Uthman ilikuwepo haja ya kuwaunganisha Waislam kwa kusoma msomo mmoja tu na katika msahafu mmoja.

  Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) ametuamrisha kuwa tutakapoona khitilafu nyingi, basi tufuate mafundisho yake na mafundisho ya Makhalifa waongofu watakaokuja baada yake.

  Na Uthman (Radhiya Llahu anhu) ni Khalifa wa tatu muongofu.

  Imam Ahmed, Ibni Majah, Attirmidhy  Naasikh na Mansukh (Aya zilizofuta na zilizofutwa)

  Kabla ya kuendelea mbele ningependa kwanza kuelezea juu ya hukmu hii ya Naasikh na Mansukh (Aya zilizofuta na zilizofutwa), na jambo hili limekubaliwa na wanavyuoni wote wa Kiislamu wa kila madhehebu.

  Mwenyezi Mungu anasema:

  مَا نَنسَخْ مِنْ آيَةٍ أَوْ نُنسِهَا نَأْتِ بِخَيْرٍ مِّنْهَا أَوْ مِثْلِهَا أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللّهَ عَلَىَ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

  “Aya yo yote tunayoifuta au kuisahauliza tunaleta iliyo bora kuliko hiyo au iliyo mfano wake. Hujui kwamba Mwenyezi Mungu Anao uweza juu ya kila kitu?”

  Al Baqarah- 106  Anasema Imam Shafi (Rahimahullah):

  “Mwenyezi Mungu hafuti hukmu isipokuwa ataleta badala yake hukmu nyingine. Mfano pale alipoifuta hukmu ya kuelekea Baytul Maqdis katika Swala kisha akaileta badala yake hukmu ya kuelekea Al Kaaba”.

  Imam Shafi akiendelea kutoa mifano alisema:

  “Mwenyezi Mungu Anasema:

  يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَسْبُكَ اللّهُ وَمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ عَلَى الْقِتَالِ إِن يَكُن مِّنكُمْ عِشْرُونَ صَابِرُونَ يَغْلِبُواْ مِئَتَيْنِ وَإِن يَكُن مِّنكُم مِّئَةٌ يَغْلِبُواْ أَلْفًا مِّنَ الَّذِينَ كَفَرُواْ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لاَّ يَفْقَهُونَ

  “Ewe Mtume (wa Mwenyezi Mungu)! Wahimize walioamini wende vitani. Wakipatikana kwenu watu ishirini wanaousubiri watashinda mia mbili (katika hao makafiri. Basi nyinyi mkiwa ishirini lazima msimame mupigane na watu miteni).

  Na kama wakiwa watu mia moja kwenu watashinda elfu moja ya wale waliokufuru, maana hao ni watu wasofahamu. (Basi watu mia katika nyinyi wasiwakimbie watu elfu katika wao)”

  Al Anfal 64 – 65

  Katika aya hizi Mwenyezi Mungu anatujulisha kuwa Waislam wanazo nguvu za Imani kiasi ambapo ishirini wanaweza kupigana na makafiri mia mbili na kwamba Mwislam mmoja anatakiwa asikimbie akipambana na makafiri kumi.

  Lakini baada ya Mwenyezi Mungu kuona kuwa upo udhaifu, Naye Subhanahu wa Taala Alielewa kuwa utakuwepo udhaifu tokea mwanzo, na hii inatokana na vita kuendelea muda mrefu, Mwenyezi Mungu Akapunguza idadi, kwa kutujulisha kuwa sasa Waislam mia moja wanaweza kuwashinda makafiri mia mbili. Muislam mmoja anatakiwa asikimbie akipigana na makafiri wawili.

  Mwenyezi Mungu anasema:

  الآنَ خَفَّفَ اللّهُ عَنكُمْ وَعَلِمَ أَنَّ فِيكُمْ ضَعْفًا فَإِن يَكُن مِّنكُم مِّئَةٌ صَابِرَةٌ يَغْلِبُواْ مِئَتَيْنِ وَإِن يَكُن مِّنكُمْ أَلْفٌ يَغْلِبُواْ أَلْفَيْنِ بِإِذْنِ اللّهِ وَاللّهُ مَعَ الصَّابِرِينَ

  “Sasa Mwenyezi Mungu amekukhafifishieni maana anajua ya kwamba kuna udhaifu (sasa) kwenu (kwa kuwa vita vimeendelea kwa mda mrefu). Kwa hivyo wakiwa watu mia moja kwenu wenye subira na wawashinde watu mia mbili kwao; na kama wakiwa elfu moja miongoni mwenu nawawashinde elfu mbili; kwa amri yaMwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri (yaani sasa wanaambiwa kila Muislam mmoja akabiliane na makafiri wawili)”.

  Al Anfal – 66  Hii ni mifano miwili katika kuisherehesha maana ya kufutwa aya na kuletwa nyingine badala yake, na inajulikana na wanavyuoni wa Madhehebu yote kuwa zipo aya zinazofutwa zikaletwa nyingine badala yake na zipo nyingine zinafutwa bila kuletwa nyingine na zipo zinazofutwa kimaandishi lakini hukmu yake inabaki nk.  Abu Jaafar At Tuwsiy ambaye ni Mzee wa Taifa la Shia katika kitabu cha Attibiyan fiy Tafsiyr Al Qur'an Juzuu ya 1 Ukurasa 13 ameeleza aina mbali mbali za kufutwa kwa aya

  Kamal u Diyn al Ataiqiy kaelezea pia katika kitabu chake Annasikh wal Mansukh.

  Muhammad Aly katika Lamahat min tariykh al Qur'an Ukurasa 222

  Wanavyuoni hawa na pia wengine wameandika juu ya Nasikh na Mansukh kama tutakavyoona kila tukiendelea mbele Inshaallah.  Hadihi zilizowababisha baadhi ya watu

  1. Ayatul Ridha a.

  2. Ayatul Rajm

  3. Hadithi ya Ibni Masaud

  4. Surat Al Hafd na Al Khala'a (الحفد والخلع)  Zipo hadithi mbili zinazowababaisha baadhi ya watu wakadhania kuwa kulikuwa na aya katika Qur'ani zikisomwa na baadaye zikaondolewa. Hadithi hizi zinajulikana kuwa ni za “Aya ya Radha-a na ya Rajm”.

  Ya kwanza; Hadithi ya Bibi Aisha iliyosimuliwa na Imam Malik inayosema:

  “Ilikuwa katika yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, ikijulikana kuharimishwa baada ya kunyonya mara kumi, ikabadilishwa kwa kunyonya mara tano na haya ndiyo yanayosomwa katika Qurani.”

  Maulamaa wanasema kuwa hadithi hii si dalili kuwa aya hii ilikuwemo ndani ya Qurani kisha ikafutwa, hasa kwa vile hadithi ni dhaifu kwa sababu ni katika hadithi zinazoitwa (Aahaad) zilizopokelewa kwa njia ya mtu mmoja tu.

  Na hata kama itakubalika kwa ajili ya mjadala, basi natija yake itakuwa hivi;

  Hadithi inasema; ‘Ilikuwa katika yaliyoteremshwa…’ na inajulikana kuwa Mwenyezi Mungu Ameteremsha wahyi mwengine usiokuwa Qurani kwa sababu Hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) na Hadith al Qudusiy pia ni katika aliyoteremshiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam), lakini si katika Qurani.

  Mwenyezi Mungu anasema:

  وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ

  Na tumekuteremshieni mauidha ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao na ili wapate kufikiri."

  An - Nahli-44

  Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam) katika hadithi iliyosimuliwa na Bukhari amesema:

  “Mimi nimeteremshiwa Qurani na nyingine iliyo mfano wake pamoja nayo”.  Na kama inavyojulikana kuwa sheria nyingi zimepokelewa kwa njia ya hadithi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swallah Llahu alayhi wa sallam).  Anasema Abu Jaafar At Tuwsiy ambaye ni Mzee wa Taifa la Shia:

  "Katika zilizofutwa usomaji na hukmu kwa pamoja ni ile riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Aisha kuwa alisema:

  “Ilikuwa katika yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu ikijulikana kuharimishwa baada ya kunyonya mara kumi, ikabadilishwa kwa kunyonya mara tano na haya ndiyo yanayosomwa katika Qurani.”  Ya pili; ni hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Umar bin Khatwaab (Radhiya Llahu anhu) kuhusu aya ya Rajm isemayo:

  “Mwenyezi Mungu amemleta Muhammad kwa haki na akamteremshia kitabu, na katika aliyoteremshiwa ni aya ya rajm (kupiga mawe), tuliisoma na kuifahamu na tukapiga mawe, ninaogopa wakati ukipita mtu anaweza kusema;

  ‘Mbona hatuioni aya ya mawe katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Ningekuwa siogopi kuwa watu watasema kuwa Umar kaongeza kitu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi ningeiandika.”

  Anasema Sheikh Al Qutby Mahmoud katika kitabu chake kiitwacho ‘Mabaahith fiy Uluum al Quraan;

  "Sisi hatuamini kuwa Umar na Aisha (Rahdiya Llahu anhum) wanaweza kusema maneno kama haya ingawaje hadithi hizi mbili zimo katika vitabu vya hadithi, kwa sababu katika vitabu vya hadithi, zimo nyingi zenye udhaifu wa Isnad.

  Hata hivyo, kama tutaijadili hadithi hii kwa ajili ya mjadala tu, pana dalili katika kauli ya Umar kuwa hayo yaliyoteremshwa si katika Qur'ani, na hii inatokana na pale alipoikamilisha kauli yake kwa kusema:

  “Ningelikuwa siogopi kuwa watu watasema kuwa Umar kaongeza kitu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi ningeiandika.”

  Kisha hii pia ni katika hadithi za ‘Aahaad’ na siyo ‘Mutawatir’ na maana ya hadith ‘Mutawaatir’ ni Hadithi iliyosemwa na wasiopungua watu kumi katika kila tabaka la wasimulizi 'Ar Ruwaat' na maana yake ni kuwa lazima wawe kumi katika tabaqa la Masahaba na kumi katika tabaqa ya Al Tabiiyn na kumi katika tabaqa la Taabea al Tabiiyn hata ifikie daraja la kuweza kukubaliwa kuwa ni katika Qurani."

  (mwisho wa maneno ya Al Qutby)  Wapo baadhi ya Maulamaa wakubwa wa Shia wanaosema kuwa aya hizi ni katika zile zilizofutwa kusoma lakini hukmu yake ikabaki, nao ni kama ifuatavyo:

  Anasema .Abu Aly Al Fadhl Attubrusy katika kuifasiri aya ya 106 ya Suta al Baqarah:

  "Kufutwa kwa aya kupo aina nyingi; ikiwemo yenye kufutwa kusomwa lakini hukmu inabaki, mfano wa aya ya Rajm."

  Muj'maa l bayan fiy tafsiyr Al Qur'an  Anasema At Tuwsiy ambaye ni maarufu kwa jina la Mzee wa Taifa la Shia:

  "Kufutwa kwa aya ndani ya Qur'ani kupo namna tatu; miongoni mwa namna hizo ni kufutwa usomaje wake na kubaki hukmu yake, mfano wa aya ya Rajm (kupigwa mawe mzinzi) nayo ni kauli isemayo: "Mtu mzima mwanamke na mtu mzima mwanamume wakizini basi wapigeni mawe vizuri ni adhabu itokayo kwa Mwenyezi Mungu.'

  Attibyan fiy tafsiyr Al Qur'an- tafsiri ya aya ya 104 Al Baqarah  Kamal Uddiyn Abdul Rahman al Ataiqiy Al Huliy katika kitabu chake 'Annasikh wal Mansukh' amesema:

  "Kuna Mansukh namna tatu; Ipo iliyofutwa maandishi ikabaki hukmu mfano wa riwaya inayosema: "Mtu mzima mwanamke na mtu mzima mwanamume wakizini basi wapigeni mawe".  Na Al Kulayni aliitaja aya ya al Rajm katika Al Kafi na alisema Aly Akbar aliyekifanyia tahakiki kitabu hicho kuwa; "Imefutwa kusomwa kwake."  Muhammad Baqer Al Majlisiy aliisahihisha riwaya ya Al Rajm akasema: "Nimeihisabu aya hii katika zile zilizofutwa."  Tulisoma namna gani katika ukusanyaji wa Qur'ani wakati wa Abubakar, Zeyd alipomkatalia Umar kupunguza herufi moja tu ya ‘Waaw’ mpaka alipoleta shahidi aliyehifadhi aliyekuwa katika waandishi wa Wahyi ambaye ni Kaab, hata hivyo Kaab, alishuhudia dhidi ya Umar (Radhiya Llahu anhum jamiy'an).  Kwa hivyo hadithi hiyo ya Umar inayohusiana na Rajm haikuwemo katika Qur'ani, Kwa sababu Umar (Radhiya Llahu anhu) mwenyewe ametamka:

  “Ningekuwa siogopi kuwa watu watasema kuwa Umar kaongeza kitu katika kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi ningeiandika.”

  Ikajulisha kuwa haikuwa katika Qurani.  Ama kuhusu hadithi ya kunyonya, hiyo ina mgongano mingi katika isnad yake na kwa ajili hiyo pia haiwezi kufikia daraja ya kuwa aya katika Qurani.  Hadithi ya Ibni Masaud (Radhiya Llahu anhu)

  Anassema mwanachuoni Mannaa'a Al Qattan:

  "Yaliyonukuliwa kutoka kwa Ibni Masaud (Radhiya Llahu anhu) si sahihi kwa
  sababu yanakwenda kinyume na Ij'maa ya umma. Anasema Imam Annawawiy katika Shar'h al Muhadhib; 'Waislamu wote wamekubalina kwa Ij'maa kuwa Muawwidhatayn; (Qul audhu birabil falaq na Qul audhu birabbin nas) na Surat al Fatihah ni katika Qurani, na atakayekanusha yeyote kati ya hizo basi keshakufuru. Na yale yaliyonukuliwa kutoka kwa Ibni Masaud (Radhiya Llahu anhu) ni batil na siyo sahihi.' Na akasema Ibni Hazm; 'Huu ni uongo aliosingiziwa Ibni Masaud, bali ni Maudhui'." Anaendelea kusema Mwanachuoni Mannaa'a al Qattan: "Na hata kama yatakuwa sahihi kwa mfano; huenda akawa Ibni Masaud hakuzisikia sura hizo kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Llahu alayhi wa sallam), ndiyo maana akaogopa kuziingiza ndani ya msahafu wake. Na kuzikataa sura hizo Ibni Masaud hakuwezi kuwa bora kupita Ij'maa ya umma huu kuwa sura hizo ni katika Qur'ani, tena zimepokelewa kwa njia Mutawaatir."

  katika kitabu chake 'Mabahith fiy Uluwm al Qur'an' uk. 136/137:

  Anasema Abdul Rahman Addamashqiy:

  "Na inayodhoofisha zadi hadithi hii ni hadithi nyingi sana sahihi tena zilizopokewa kwa njia Mutawatir kutoka kwa usomaji wa Aaswim kutoka kwa Zar kutoka kwa Hubeysh kutoka kwa huyu Abdillahi bin Masaud (Radhiya Llahu anhu), na katika hadithi hizo za Ibni Masaud imo Surat al Fatiha na zimo pia Qul audhu mbili. Na kama kauli hiyo aliitoa kweli Ibni Masaud, basi itakuwa ni wakati ule kabla haijapatikana Ijmaa ya Waislamu."

  Amesema Imam An Nawawiy:

  "Wamekubaliana Waislamu wote (Ij'maa) kuwa Qul audhu mbili na Al Fatiha na sura zote zilizoandikwa katika msahafu ni Qur'ani, na mwenye kuzikanusha zozote kati ya hizo keshakufuru, na yaliyonukuliwa kutoka kwa Ibni Masaud ni batil na wala siyo sahihi."

  Al Maj'muu – Sharhi ya tahdhiyb  Sura ya Al Khalaa na Al Hafd

  Wanadai Manasara kuwa zipo Sura mbili zilizokuwemo ndani ya Qurani zikaondolewa, na sura hizo ni Surat al Khalaa na Surat Al Hafd.

  Na Sura hizo zinasema hivi:

  اللهم إنا نستعينك و نستهديك و نستغفرك و نتوب إليك و نؤمن بك و نتوكل عليك و نثني عليك الخير كله .نشكرك و لا نكفرك . ونخلع و نترك من يفجرك .اللهم أياك نعبد و لك نصلي و نسجد .و إليك نسعى و نحفد و نرجورحمتك و نخاف عذابك الجد بالكفار ملحق

  Na imepokelewa kuwa baadhi ya Masahaba walikuwa wakizisoma aya hizo katika Qunut.

  Na katika riwaya nyingine kuwa Umar bin Khatwaab alikuwa akizisoma sura hizo ndani ya Qunut baada ya kurukuu akisema:

  بسم الله الرحمن الرحيم. اللهم إنا نستعينك ونستغفرك. ونثني عليك ولا نكفرك. ونخلع ونترك من يفجرك. بسم الله الرحمن الرحيم. اللهم إياك نعبد. ولك نصلي ونسجد. وإليك نسعى ونحفد. نرجو رحمتك ونخشى عذابك. إن عذابك الجد بالكافرين ملحِق.

  Jawabu:

  Hii ni dua ya Qunut ambayo Ubay aliiandika ndani ya msahafu wake, na inajulikana kuwa Waislamu hawasomi Qur'ani ndani ya Qunut. Isitoshe, hapana ushahidi wowote wa hadithi sahihi inayokubalika kuwa kulikuwa na sura kama hizi ndani ya Qurani.  Kama tulivyotangulia kusoma ni kuwa wakati Wahyi ukiteremka, Masahaba walikuwa wakiiandika Qur'ani ndani ya karatasi zao na ndani ya misahafu yao, na kwa vile kulikuwa na upungufu mkubwa wa sehemu za kuandikia, wakawa humo wakiandika pia dua zao na mara nyingine wakiandika hata hadithi za Mtume (Swallah Llahu alayhi wa sallam), na haya yaliendelea mpaka ulipofika wakati wa Ukhalifa wa Uthman (Radhiya Llahu anhu) wakati Waislamu walipoamua kwa Ij'maa kuiandika Qurani yote ndani ya msahafu mmoja na kuichoma moto iliyobaki.

  Hapana riwaya sahihi hata moja ambayo ndani yake Kaab ametamka kuwa dua zile ni katika Qurani tukufu.

  Anasema Azzamakhshariy katika Al Burhan:

  "Imepokelewa riwaya kuwa Ubay bin Kaab ameiandika dua hii ndani ya msahafu wake na kwamba ameandika pia ndani ya msahafu wake mengine yasiyokuwa Qur'ani."

  Al Burhan fiy Ulum al Qur'an2/132

  Isitoshe, zimepokelewa riwaya nyingi sana kutoka kwa Ubay juu ya usomaji wake wa Qur'ani kutoka kwa Naafea na Ibni Kathiyr na Abu Amru na wengi wengineo, na katika misomo yote hiyo hamna hata riwaya moja inayosema kuwa ndani yake pana sura ya Al Khalaa au sura ya Al Hafd.

  Imepokelewa kuwa Abul Hassan Al Ash'ary amesema:

  "Niliusoma msahafu wa Anas katika mji wa Basra kwa wanawe, nikauona uko sawa na misahafu mingine yote."

  Na inajulikana kuwa watoto wa Anas walikuwa na msahafu wa baba yao aliouandika huku akisomewa na Ubay bin Kaab (Radhiya Llahu anhu).  Na hii ni dalili nyingine kuwa Al Khalaa na Al Hafd hazikuwa sura, bali zilikuwa dua zilizokuwa
  zikisomwa katika Qunut.

   Current date/time is Fri Jan 18, 2019 1:07 pm