.


  Miujiza Ya Qur'aan

  Share
  avatar
  BESTY
  Admin

  Posts : 3
  Join date : 2010-08-28
  Location : Here

  Miujiza Ya Qur'aan

  Post  BESTY on Sun Aug 29, 2010 6:27 pm

  Baadhi ya Dalili Zenye Kuonyesha Ukweli Wa Uislamu

  Sehemu ya 1

  Mwenyezi Mungu Amemuauni Mtume Wake wa mwisho, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kumpa miujiza mingi na dalili nyingi zinazothibitisha kuwa yeye ni Mtume wa kweli aliyetumwa na Mwenyezi Mungu. Kadhalika, Allaah Amekisaidia kitabu Chake cha mwisho kuteremshwa, Qur-aan Tukufu, kwa miujiza mingi inayodhihirisha wazi kuwa Qur-aan hii ni neno khalisi la Allaah Aliloliteremsha, na kwamba, haikutungwa na mwanaadamu yeyote. Sehemu hii inaeleza baadhi ya dalili hizo.

  (1) Miujiza ya Kisayansi Iliyo Ndani ya Qur-aan Tukufu  Qur-aan ni neno khalisi la Mwenyezi Mungu, aliloteremsha kwa Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kupitia kwa Malaika Jibriyl.

  Ilikaririwa na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye naye aliwasomea Maswahaba wake. Wao pia, waliikariri, wakaiandika na wakaidurusu pamoja na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). zaidi ya hivyo, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiitalii Qur-aan pamoja na Malaika kwa kila mwaka mara moja ilhali katika mwaka wake wa mwisho humu duniani, alifanya hivyo mara mbili. Tangu wakati Qur-aan ilipoteremshwa hadi hivi leo, kumekuwa na idadi kubwa ya Waislamu walioikariri Qur-aan, herufi kwa herufi. Baadhi yao wamemudu kuikariri Qur-aan yote wakingali katika umri wa miaka kumi tu. Katika kipindi cha karne zote hizi, hakuna hata herufi moja ya Qur-aan iliyobadilishwa.

  Qur-aan, ambayo iliteremshwa mnamo karne kumi na nne zilizopita, ilitoa taarifa ambazo hivi karibuni tu ndio zimegunduliwa au kuhakikishwa na wanasayansi. Jambo hili linathibitisha pasi na shaka kuwa Qur-aan ni neno khalisi la Mwenyezi Mungu Alilomteremshia Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kwamba haikutungwa na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au mwanaadamu yeyote.

  Hili pia linadhihirisha kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Mtume wa kweli aliyetumwa na Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka yoyote hakuna yeyote wa karne kumi na nne zilizopita aliyeweza kuzijua taarifa hizi ambazo ni hivi karibuni tu zimegunduliwa au kuhakikishwa kwa kutumia zana za kisasa na njia za hali ya juu za kisayansi. Baadhi ya mifano inafuata hapa chini.
  avatar
  BESTY
  Admin

  Posts : 3
  Join date : 2010-08-28
  Location : Here

  Re: Miujiza Ya Qur'aan

  Post  BESTY on Sun Aug 29, 2010 6:34 pm

  Maelezo ya Qur-aan Juu ya Ukuaji wa Kiinitete cha Mwanaadamu

  Ndani ya Qur-aan Tukufu, Mwenyezi Mungu Anaeleza hatua za ukuaji wa kiinitete cha mwanaadamu:

  “Na kwa yakini Tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo. Kisha Tukamjaalia awe tone ya mbegu ya uzazi katika kalio madhubuti. Kisha Tukaiumba tone kuwa ‘Alaqah (ruba, kitu chenye kusubirishwa, na tone la damu), na Tukaiumba ‘Alaqah kuwa Mudhwghah (kitu kilichotafunwa, yaani pande la nyama)…”[1](Qur-aan 23:12-14)

  Kwa uhakika, neno la Kiarabu, ‘Alaqah lina maana tatu:

  1) ruba,
  2) kitu chenye kusubirishwa, na
  3) tone la damu.


  Katika kulinganisha ruba na kiinitete katika hatua ya ‘alaqah, tunaona kuna mlingano baina ya viwili hivi,[2] kama tunavyoweza kuona katika umbo namba 1. Pia, kiinitete katika hatua hii hupata chakula kutoka katika damu ya mama yake, sawa sawa na ruba, ambaye hujipatia chakula chake kutoka katika damu ya wengine.[3]
  ________________________________________________________________________

  1Tafadhali, tambua kwamba kilicho baina ya fungua na funga semi hizi katika kitabu hiki ni tafsiri tu ya Qur-aan. Si Qur-aan yenyewe ambayo iko katika lugha ya Kiarabu
  2 The Developing Human, Moore and Persaud, 5th ed., p.8.
  3 Human Development as Described in the Qur-aan and Sunnah, Moore and others, p.36.

  ________________________________________________________________________

  Umbo na. 1: Michoro yenye kufafanua ulinganifu wa muonekano kati ya ruba na kiinitete cha mwanaadamu katika hatua ya ‘alaqah. (Mchoro wa ruba kutoka katika kitabu Human Development as Described in the Qur-aan and Sunnah, Moore na wengine, uk. 37, uliobadilishwa kidogo kutoka katika IntegratedPrinciples of Zoology, Hickman na wengine. Mchoro wa kiinitete kutoka katika Developing Human, Moore na Persaud, 5th ed., uk. 73.)

  Maana ya pili ya neno ‘alaqah ni “kitu chenye kusubirishwa.” Hicho ndicho tunachoweza kukiona katika maumbo namba 2 na 3, kusubirishwa kwa kiinitete kikiwa katika hatua ya ‘alaqah, tumboni mwa mama.

  ________________________________________________________________________

  Umbo na. 2: Katika mchoro tunaweza kuona kusubirishwa kwa kiinitete kikiwa katika hatua ya ‘alaqah tumbo la uzazi (mji wa mimba) la mama. (The Developing Human, Moore na Persaud, 5th ed., uk. 66.)

  ________________________________________________________________________

  Umbo na 3: Katika Fotomaikrograf (Photomicrograph) hii, tunaweza kuona kusubirishwa kwa kiinitete (alama Cool wakati wa hatua ya ‘alaqah (kadiri ya umri wa siku 15) katika tumbo la uzazi la mama. Kipimo khalisi cha kiinitete ni kadiri ya milimita 0.6. (The Developing Human, Moore, 3rd ed., uk. 66, Kutoka katika Histology, Leeson and Leeson.)

  Maana ya tatu ya neno ‘alaqah ni “tone la damu.” Tunakuta kwamba muonekano wa sehemu ya nje ya kiinitete na kifuko chake katika hatua ya ‘alaqah unashabihiana na ulewa tone la damu. Hii ni kutokana na kuwepo kwa kiasi kikubwa cha damu iliyomo ndani ya kiinitete wakati wa hatua hii[4](angalia umbo na. 4). Kadhalika, katika hatua hii, damu iliyo ndani ya kiinitete haizunguki mpaka mwishoni mwa wiki ya tatu. [5]

  Hivyo, katika hatua hii, kiinitete ni kama tone la damu.

  4 Humad Development as Described in the Qur-aan and Sunnah, Moore na wengine, uk. 37-38
  5 The Developing Human, Moore na Persaud, 5th ed., uk. 8

  ________________________________________________________________________

  Umbo na. 4: Mchoro wa muundo wa kiasili wa mshipa wa damu wa moyo ndani kiinitete katika hatua ya ‘alaqah. Muonekano wa nje wa kiinitete na kifuko chake unalandana na ule wa tone la damu kutokana na kuwepo kwa kiasi kingi cha damu kiuwiano ndani ya kiinitete. (The Developing Human, Moore, 5th ed. p.65)

  Hivyo, maana tatu za neno ‘alaqah linaendana sawia na maelezo juu ya kiinitete katika hatua ya ‘alaqah. Baada ya hapo, Aayah imetaja kuwa inafuata hatua ya Mudhwghah. Maana ya neno la Kiarabu, Mudhwghah, ni “kitu kilichotafunwa.” Ikiwa mtu atatafuna kipande cha ubani mdomoni mwake kisha akakilinganisha na kiinitete kilicho katika hatua ya Mudhwghah, tunaweza kupata jibu kuwa kiinitete katika hatua ya Mudhwghah kinalandana kimandhari na kitu kilichotafunwa. Hii ni kwa sababu ya somiti (somites) nyuma ya kiinitete ambayo "kwa namna fulani inafanana na alama za meno katika kitu kilichotafunwa." (angalia umbo namba 5 na 6)

  ________________________________________________________________________

  Umbo namba. 5: Picha ya kiinitete chenye umri wa siku-28 katika hatua ya Mudhwghah. Katika hatua hii, kiinitete kinafanana na kitu kilichotafunwa, kwa sababu somiti (somites) zilizo nyuma ya kiinitete, kwa namna fulani zinalandana na alama za meno katika kitu kilichotafunwa. Urefu khalisi wa kiinitete ni milimita 4. (The Developing Human, Moore and Persaud, 5th ed., uk. 82, kutoka kwa Profesa Hideo Nishimura, Kyoto University, Kyotro, Japan.)


  Umbo namba 6: Ukilinganishwa muonekano wa kiinitete katika hatua ya Mudghah na kipande cha ubani kilichotafunwa, tutakuta mfanano baina ya viwilio hivyo.
  A) Mchoro wa kiinitete katika hatua ya Mudhwghah. Hapa tunaweza kuona somiti (somites) nyuma ya kiinitete ambazo zinaonekana kama alama za meno (The Developing Human, Moore and Persaud, 5th ed., uk. 79)

  B) Picha ya kipande cha ubani uliotafunwa

  Ingewezekana vipi kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuyajua yote haya mnamo karne kumi na nne zilizopita, ilhali wanasayansi wameyagundua hivi karibuni tu, tena kwa kutumia vifaa vya vya kisasa na darubini zenye nguvu , ambavyo vyote havikuwepo katika zama hizo?

  Hamm na Leeuwenhoek walikuwa wanasayansi wa kwanza kuchunguza chembe hai za manii ya mwanaadamu (spermatozoa) mnamo mwaka 1977, kwa kutumia darubini iliyofanyiwa mabadiliko (zaidi ya miaka 1,000 baada ya Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)). Kimakosa, walidhani kuwa chembe hai ya manii ilikuwa na mwanaadamu mdogo sana aliyefanyika kabisa, ambaye alikua baada ya kuwekwa katika eneo la viungo vya uzazi vya mwanamke. [6]

  Profesa Keith L. Moore ni mmojawapo wa wanasayansi mashuhuri wenye kuheshimika katika uwanja wa anatomia (sayansi inayohusu mwili na viungo vyake jinsi vilivyo) na embriolojia (taaluma ya maisha ya kiinitete), tena ni mwandishi wa kitabu kilichoitwa The Developing Human ambacho kimetafsiriwa katika lugha nane. Kitabu hiki ni kazi ya rejea ya kisayansi na kilichaguliwa na kamati maalumu katika nchi ya Marekani kuwa ni kitabu bora kilichotungwa na mtu mmoja. Dk. Keith Moore ni Profesa wa heshima (baada ya kustaafu) wa anatomia na Biolojia ya Chembe Hai katika Chuo Kikuu cha Toronto, huko Toronto, Kanada. Hapo alikuwa Mkuu Mshiriki wa Sayansi ya Msingi (Basic Sciences) katika Kitivo cha Sayansi ya Tiba na kwa miaka 8 alikuwa Mwenyekiti wa Idara ya Anatomia. Mwaka 1984 alipokea tuzo ya aina yake kabisa iliyotolewa katika fani ya anatomia nchini Kanada, iliyoitwa Tuzo ya J.C.B. Grant kutoka Chama cha Wana-Anatomia wa Kanada. Ameongeza vyama vingi vya kimataifa, kama vile Chama cha Wana-Anatomia wa Kanada na Marekani na Baraza la Muungano wa Sayansi za ki-Biolojia.

  Mnamo mwaka 1981, wakati wa Mkutano wa Saba wa Masuala ya Madawa jijini Dammaam, Saudi Arabia, Profesa Moore alisema: “Imekuwa ni furaha kubwa kwangu kusaidia ufafanuzi wa kauli zilizo katika Qur-aan kuhusu ukuaji wa mwanaadamu. Ni dhahiri kwangu kuwa kauli hizi ni lazima zitakuwa zimetoka kwa Mwenyezi Mungu na kumfikia Muhammad kwani elimu hii yote haikugunduliwa mpaka baada ya karne nyingi baadaye. Hili linanidhihirishia kuwa ni hakika kwamba Muhammad ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu.”[7] Matokeo yake, Profesa Moore aliulizwa swali hili: “Je, Hii inamaanisha kuwa unaamini kwamba Qur-aan ni neno la Mwenyezi Mungu?” Akajibu: “Sioni ugumu wa kukubali hivyo.” [8]

  Katika mkutano mmojawapo, Profesa Moore alisema: “…Kwa sababu ufanyikaji wa hatua za kiinitete cha mwanaadamu ni changamani (una sehemu na tabia nyingi) kwa sababu ya mabadiliko endelevu wakati wa makuzi, imependekezwa kuwa mfumo mpya wa uanishaji unaweza kuelezwa kwa kutumia maneno yaliyotumika katika Qur-aan na Sunnah. Muundo uliopendekezwa ni rahisi, wa kufahamika na unakubaliana na elimu ya zama hizi ya kiembriolojia. Usomaji wa makini wa Qur-aan na Hadiyth katika miaka minne iliyopita umefunua mfumo kwa ajili ya uainishaji wa viinitete vya kibinaadamu ambao ni wa kustaajabisha tangu uliponukuliwa katika karne ya saba baada kuzaliwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam) (7 M). Ingawa Aristotle, mwanzilishi wa elimu ya embriolojia alitambua kuwa viinitete vya kuku vilikua hatua kwa hatua, kutokana na uchunguzi wake juu ya mayai ya kuu katika karne ya nne kabla ya kuzaliwa Nabii ‘Iysa (‘Alayhis Salaam), hakutoa maelezo yoyote kuhusu hatua hizo. Kadiri ijulikanavyo katika historia ya embriolojia, kulikuwa na ujuzi kidogo tu juu ya kuwepo hatua na uainishaji wa viinitete vya kibinaadamu mpaka karne ya ishirini. Kwa minajili hiyo, maelezo juu ya kiinitete cha kibinaadamu kutoka ndani ya Qur-aan hayawezi kuwa yameegemea elimu ya kisayansi katika karne ya saba. Khitimisho pekee lenye maana ni: maelezo haya yalifunuliwa kwa Muhammad kutokea kwa Mwenyezi Mungu. Asingeliweza kuyajua maelezo hayo mwenyewe kwa sababu alikuwa asiyesoma na kabisa hakuwa na mafunzo ya kisayansi.” [9]

  [1] Tafadhali, tambua kwamba kilicho baina ya fungua na funga semi hizi katika kitabu hiki ni tafsiri tu ya Qur-aan. Si Qur-aan yenyewe ambayo iko katika lugha ya Kiarabu
  [2] The Developing Human, Moore and Persaud, 5th ed., p.8.
  [3] Human Development as Described in the Qur-aan and Sunnah, Moore and others, p.36.
  [4] Humad Development as Described in the Qur-aan and Sunnah, Moore na wengine, uk. 37-38
  [5] he Developing Human, Moore na Persaud, 5th ed., uk. 8
  [6] The Developing Human, Moore na Persaud, 5th ed., uk. 9
  [7] Chanzo cha maoni haya ni This is the Truth (Huu ndio Ukweli) (mkanda wa video). Tembelea www.islam-guide.com/truth kwa ajili ya kupata nakala ya mkanda huo au kuangalia video fupi ya maoni ya Profesa Keith Moore iliyounganishwa na kompyuta kuu (online) au (Bonyeza hapa ).
  [8] This is the Truth (mkanda wa video)
  [9] This is the Truth (mkanda wa video ). Angalia rejeo namba 7

   Current date/time is Fri Jan 18, 2019 12:34 pm